Mvutano wa kijografia, vita na migogoro inayoendelea katika Mlango Bahari wa Hormuz kati ya Iran na washirika wake imeleta madhara makubwa katika uchumi duniani. Bei za mafuta zimepanda na hivyo kusababisha mfumuko mkubwa wa bei kwa bidhaa na huduma muhimu.
Katika baadhi ya nchi, hali hii imesababisha kuwepo kwa mtikisiko wa kiuchumi ikiwemo katika mataifa ya jirani. Hata hivyo, Tanzania yetu ina nafasi ya kujitofautisha, Historia yetu ya amani na utulivu inatupa fursa ya kuwa kisiwa cha amani na utulivu hapa duniani.
Watanzania wameendelea kuwa imara na kudumu kama misingi hiyo iliyojengwa tangu kuasisiwa kwa Taifa letu, tumeweza kwa sababu tumendelea kuepuka chuki, migawanyiko na siasa za ubinafsi. Umoja wa kitaifa ndio silaha yetu yenye nguvu zaidi katika kipindi hiki kigumu.
Tukiendeleza na kudumisha umoja, inakuwa rahisi kushirikiana na Serikali katika kutatua changamoto zetu wenyewe. Serikali haiwezi kufanya lolote bila ushirikiano wa wananchi. Tunapoungana, tunaweza kushughulikia kila Jamabo linalohitaji nguvu ya pamoja. Aidha, umoja huu unatuwezesha kuimarisha uzalishaji katika Sekta zote ikiwemo kilimo chetu, kukuza biashara ndogondogo na kulinda amani yetu. Tunapogawanyika, adui yetu mkubwa ni sisi wenyewe.
Wanaume na wanawake wa Tanzania, vijana na wazee, tuwe kitu kimoja. Tuache maneno ya chuki na kugawanya taifa. Amani si maneno matupu, ni chombo cha maendeleo. Tuilinde umoja wetu kama tulivyolinda taifa letu tangu uhuru. Katika wakati huu wa migogoro ya kimataifa, umoja wetu ndio utakaotufanya tuibuke washindi.
Tuishi kwa amani. Tuishi kwa umoja. Tanzania kwanza!