DAR ES SALAAM — Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Othman Chande amesema uchunguzi wa kitaalamu wa kidijitali uliofanywa na Tume ya Uchunguzi umebaini kuwa baadhi ya picha na video zilizosambazwa sana kwenye mitandao ya kijamii wakati wa vurugu zilizohusiana na Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 zilihaririwa kwa kutumia akili unde (AI) ili kuonesha taswira ya mauaji makubwa na vifo vya watu wengi.
Jaji Chande alisema hayo leo Aprili 23, 2026 Ikulu alipokuwa akiwasilisha matokeo ya uchunguzi wa tume kwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Alisema wataalamu wa uchunguzi wa kidijitali waliotumika na tume waliweza kutofautisha kati ya taarifa halisi na zilizohaririwa kwa kutumia uchambuzi maalumu wa kitaalamu.
“Moja ya mifano ni picha iliyokuwa ikisambazwa mara kwa mara ikionyesha miili ndani ya mifuko ya bluu ikidaiwa kuzikwa kwenye makaburi ya pamoja. Uchunguzi umebaini kuwa picha hiyo hiyo imetumika katika maeneo mbalimbali duniani,” alisema Jaji Chande.
Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo wa tume, uchunguzi ulitegemea ushahidi na taarifa zilizokusanywa kutoka vyanzo mbalimbali kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya uthibitishaji wa ushahidi vinavyotumika katika tume za uchunguzi.
Alisema mfumo huo ulihakikisha ushahidi uliokusanywa ulikuwa wa kuaminika, unaoweza kuthibitishwa na wa kina.
Jaji Chande alisema tume ilikusanya picha 450 na video 880 kutoka vyanzo mbalimbali wakati wa uchunguzi.
“Vifaa hivyo vilijumuisha taarifa zilizosambazwa mtandaoni mara kwa mara, ushahidi kutoka kwa mashahidi, taarifa kutoka vyombo vya usalama pamoja na taarifa kutoka taasisi za habari na mitandao ya kijamii,” Jaji Chande.
Alisema uchunguzi huo wa kidijitali ulikuwa sehemu ya uchunguzi mpana uliolenga kuthibitisha uhalisia wa taarifa zilizosambazwa wakati na baada ya vurugu zilizohusiana na Uchaguzi Mkuu wa 2025.