Wakati dunia ikipambana na myumbo wa kiuchumi na migogoro ya kisiasa, Tanzania imeendelea kuwa kisiwa cha matumaini na utulivu. Wachambuzi wanasema “Amani ni mtaji” na mafanikio tunayoyaona leo katika elimu, afya na michezo yanathibitisha kauli hiyo. Si miujiza, bali ni matunda ya amani na utulivu wa kisiasa unaoendelea nchini.

Serikali ya Awamu ya Sita imefanya mapinduzi makubwa katika sekta ya elimu kwa kuwekeza kwenye ujuzi wa vitendo badala ya vyeti tu. Ujenzi wa vyuo 64 vya VETA katika wilaya mbalimbali, pamoja na chuo kimoja cha mkoa wa Songwe, ni mkakati wa makusudi wa kuwapa vijana silaha ya kujiajiri. Waziri wa Elimu, Profesa Adolf Mkenda, alisisitiza kwamba “elimu na ujuzi ndio mpango mzima.” Mkakati huu unaungwa mkono na mikopo ya asilimia 10 ya halmashauri kwa vijana, wanawake na wenye ulemavu.

Faida za amani zinagusa pia sekta ya afya na ustawi wa watumishi. Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha kuwa Tanzania imepanda katika kipimo cha Afya kwa Wote kutoka alama 38 hadi 43. Miradi ya nyumba za watumishi imepunguza mzigo wa maisha kwa wafanyakazi wa umma. Haya yote yasingewezekana katika mazingira ya vurugu, kwani fedha za maendeleo zingetumika tu kukarabati miundombinu iliyoharibiwa na ghasia.

Zaidi ya hayo, amani imefungua milango ya diplomasia ya michezo. Mchambuzi Rahel Pallangyo anabainisha kuwa utulivu wa nchi ndio uliotupa heshima ya kuandaa mashindano makubwa kama AFCON 2027. Wawekezaji wa kimataifa na mashirikisho ya michezo hawawezi kupeleka fedha zao katika nchi isiyo na usalama.

Dira ya Taifa ya 2050, ambayo inalenga kurasimisha ardhi na kuwapa vijana umiliki, itatimia tu ikiwa tutaendelea kushikamana na amani. Maendeleo yote kuanzia VETA, afya bora, hadi viwanja vya michezo yanategemea kitu kimoja tu: amani.

Mfanyabiashara Amina Ali kutoka Kariakoo anasema, “Amani ndiyo kila kitu. Hapa biashara inakwenda vizuri kwa sababu hakuna maandamano yanayovuruga. Vijana wasichague fujo, waende VETA wajifunze ustadi wa biashara au umeme. Hiyo ndiyo fursa halisi.”

Mwalimu Juma Maleko kutoka Mbezi anaongeza, “Ninafurahia sana vyuo vya VETA vinavyojengwa. Mtoto wangu wa kike anaweza kujifunza ustadi wa kilimo au tourism hapa karibu badala ya kukimbilia mjini ovyo. Amani inatupa nafasi ya kupanga maisha yetu bila hofu.”

Naye Masato Nyamhanga ambaye ni fundi Umeme kutoka Chanika anahitimisha, “Tulikuwa tunasubiri miaka mingi. Sasa naona fursa za VETA zinakaribia. Lakini kama kuna ghasia, wawekezaji wataondoka na AFCON 2027 itakwenda. Vijana tuchague amani na kazi, si kelele za mitandaoni.”