Dar es Salaam – Kuna vijana wengi katika jiji letu la Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla wanaopambana na uraibu wa pombe na madawa ya kulevya. Lakini kuna hadithi moja ya kutia moyo inayotoka kwa kijana anayeomba kutotajwa jina (kwa kuogopa unyanyapaa). Anasema chess ilikuwa “escape” yake yaani njia ya kutoroka kwenye ulevi sugu na hatimaye kurejea kwenye maisha yenye tija.

“Nilikuwa mlevi mkubwa haswaa,” anasema kwa sauti ya utulivu. “Pombe ilikuwa imenichukulia kila kitu kama familia, marafiki, na hata matumaini yangu. Nilikuwa nimeacha shule na niliishi maisha ya ovyo kama chokoraa.” Lakini siku moja wakati alipokuwa akicheza na kompyuta yake ya zamani, aligundua programu rahisi ya kufundisha chess. Alianza kujifunza hatua kwa hatua. “Nilianza kucheza peke yangu nyumbani. Chess ilinifanya nisau pombe. Badala ya kwenda kunywa, nilikaa mbele ya skrini nikihesabu moves na kujaribu kushinda.”

Polepole, uzoefu wake ulikua. Kutoka kucheza peke yake kwenye kompyuta, alianza kutafuta wachezaji wengine. Alikutana na vikundi vya wachezaji wa chess katika maeneo kama Mikocheni, Kinondoni na hata Don Bosco Upanga. “Nilipoanza kucheza na wengine, nilijiona ninaweza. Chess ilinifundisha nidhamu, uvumilivu na kufikiri mbele.”

Leo, kijana huyu amecheza maelfu ya michezo ambapo mingi ni mtandaoni na mingine juu ya meza halisi (over the board). Amerejea shuleni na sasa anafanya kazi ya kuajiriwa. “Nimepata maisha mazuri. Sina haja ya pombe au kilevi chochote tena. Chess ilikuwa silaha yangu dhidi ya ulevi,” anasema kwa kujiamini.

Anashauri vijana wenzake Tanzania: “Jifunzeni chess. Si mchezo tu wa burudani, bali ni zana ya maisha. Inakufundisha kushinda changamoto, kutafuta fursa na kujenga maisha bora kuliko kushinda mtandaoni kupiga porojo na kuiponda serikali. Usikae na uraibu au mawazo hasi, Tumia akili yako kama nilivyofanya,linda amani yako na usiingie kwenye makundi rika mabaya. Kuna programu nyingi za bure mtandaoni na vilabu vya chess hapa Dar es Salaam. Anza leo, na uone jinsi maisha yatakavyobadilika.”

Hadithi hii inaonyesha nguvu ya michezo ya akili katika kupambana na uraibu na kuleta maendeleo. Chess si kwa wataalamu tu, bali ni kwa kila mtu anayetaka kujenga mustakabali mzuri. Vijana wa Tanzania, fanyeni chess kuwa sehemu ya maisha yenu na mtaona mafanikio yanakuja.