Na Madam Lolla
Watanzania wameaswa kuendelea kulinda na kudumisha amani na utulivu wa nchi, ambao uliasisiwa na viongozi waasisi wa Taifa, ili kuhakikisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi yanaendelea kuimarika.
Wadau mbalimbali wa maendeleo wamesema kuwa amani ni nguzo muhimu ya ustawi wa taifa, na kwamba misingi iliyowekwa na waasisi wa Tanzania imeifanya nchi kuwa kisiwa cha amani barani Afrika kwa miaka mingi.
Imeelezwa kuwa viongozi waasisi wa Taifa akiwemo Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Rais wa kwanza wa Tanganyika pamoja na Sheikh Abeid Amani Karume, Rais wa kwanza wa Zanzibar, waliweka msingi wa mshikamano, umoja na kuheshimiana miongoni mwa Watanzania bila kujali tofauti za kabila, dini au maeneo wanakotoka, ambapo msingi huo umeendelea kuwa chachu ya utulivu na maendeleo ya nchi.
Aidha, Watanzania wamehimizwa kuendelea kuenzi maadili ya taifa kwa kuepuka vitendo vinavyoweza kuchochea migogoro, chuki au mgawanyiko katika jamii, hasa kupitia matumizi ya mitandao ya kijamii.
Wachambuzi wa masuala ya kijamii wamesema kuwa kulinda amani ni jukumu la kila mwananchi, kwani mazingira ya utulivu huchochea uwekezaji, biashara na ustawi wa wananchi.
“Tunapaswa kuendelea kuilinda amani tuliyoachiwa na waasisi wa Taifa letu, kwani bila amani hakuna maendeleo,” amesema Bi. Rukia Ramadhani, mdau wa maendeleo kutoka Ilala, mkoani Dar es Salaam.
Naye, Christopher James, mdau wa maendeleo kutoka Mkoa wa Pwani amesema ni muhimu kwa kizazi cha sasa na kijacho kuendelea kuenzi misingi ya umoja, uzalendo na mshikamano ili kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa mfano wa amani na utulivu katika ukanda wa Afrika.
Wadau hao wamesisitiza kuwa kwa kushirikiana katika kulinda amani, Watanzania wataweza kuendeleza jitihada za kujenga taifa lenye maendeleo, ustawi na fursa kwa wananchi wote.