DODOMA, Tanzania
Rais wa Kenya, Mhe. William Ruto amesema uhusiano kati ya Kenya na Tanzania haujajengwa tu juu ya ujirani au ushirikiano wa kiuchumi, bali unatokana na undugu wa kihistoria unaowaunganisha wananchi wa nchi hizo mbili.
Akilihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma Mei 5, 2026, Rais Ruto alieleza kuwa ziara yake nchini Tanzania inaashiria kuimarika kwa uhusiano wa kidiplomasia na mshikamano wa kikanda kati ya mataifa hayo mawili.
“Niko hapa si kwa sababu sisi ni majirani, au marafiki, au washirika kwenye masuala mbalimbali, bali ni kwa sababu sisi ni ndugu,” alisema Ruto, akisisitiza msingi wa uhusiano wa kihistoria, kijamii na kiuchumi unaozidi kuimarika kati ya Kenya na Tanzania.
Aidha, amemshukuru mwenyeji wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, kwa ukaribisho na mapokezi mazuri aliyopata tangu kuwasili nchini, akisema hali hiyo inaakisi ukarimu wa Watanzania na dhamira ya kuendeleza ushirikiano wa karibu kati ya mataifa hayo.
Alieleza kuwa ziara yake ni mwendelezo wa juhudi za viongozi wa Afrika Mashariki kuimarisha mahusiano ya kisiasa na kiuchumi, akirejea ziara ya Rais Samia nchini Kenya mwaka 2021 kama msingi wa ushirikiano wa sasa.
Awali, Spika wa Bunge, Mussa Zungu, alimkaribisha Rais Ruto kwa heshima kubwa, akibainisha kuwa yeye ni Rais wa pili wa Kenya kuhutubia Bunge hilo baada ya Daniel Arap Moi mwaka 2002.
Spika Zungu alisema ujio wa Rais Ruto ni ishara ya kuimarika kwa uhusiano wa kidugu na kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa mabunge katika kukuza maendeleo ya kikanda.
Hotuba ya Rais Ruto imekuja wakati ambapo nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zinaendelea kuimarisha juhudi za ujumuishaji wa kiuchumi, biashara ya mipakani na maendeleo ya pamoja.
Ziara hiyo pia inaangazia dhamira ya viongozi wa kikanda kuendeleza amani, utulivu na ustawi wa wananchi kupitia ushirikiano wa karibu katika sekta mbalimbali za maendeleo.