Wananchi kutoka maeneo mbalimbali nchini wameeleza kuwa mazungumzo, kuheshimiana na kujenga maridhiano ni nguzo muhimu zinazoweza kuimarisha amani na mshikamano wa kitaifa, hususan katika nyakati ambazo jamii inahitaji umoja zaidi ili kusonga mbele kimaendeleo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi hao wamesema Tanzania imejengwa juu ya misingi ya amani na utulivu, hivyo ni muhimu kuendelea kudumisha utamaduni wa kusikilizana na kutatua tofauti kwa njia ya mazungumzo badala ya migogoro.

John Mushi, ambaye ni Mkazi wa Kigamboni, Dar es Salaam amesema kuwa mazungumzo yana nafasi kubwa katika kujenga uelewano ndani ya jamii.
“Tanzania imebarikiwa kuwa na watu wa tamaduni na mitazamo tofauti, lakini tunapokaa pamoja na kuzungumza kwa heshima tunapata suluhu. Kupitia mazungumzo na maridhiano, nchi yetu inaweza kusonga mbele ikiwa imara zaidi,” amesema Mushi

Naye Asha Abdallah, mkazi wa Kisasa, Dodoma, amesema kuwa maridhiano yanasaidia kuimarisha mshikamano wa wananchi na kulinda amani ya taifa.
“Amani ya nchi ni jukumu la kila mmoja wetu. Tukijifunza kusikilizana na kuheshimiana hata pale tunapotofautiana, tunaijenga Tanzania yenye umoja na maendeleo,” amesema Asha.

Kwa upande wake, Kevin Shija, mfanyabiashara kutoka Nyegezi, Mwanza amesema kuwa utulivu na amani vinasaidia kukuza shughuli za kiuchumi na kuimarisha maisha ya wananchi.

“Biashara na uwekezaji vinahitaji mazingira ya utulivu. Ndiyo maana maridhiano na mazungumzo ni muhimu sana, kwa sababu yanajenga mazingira ya kuaminiana na kuifanya Tanzania iwe imara zaidi,” amesema Shija.

Wananchi hao wameeleza kuwa misingi ya amani na umoja iliyoasisiwa na viongozi wa awali wa taifa bado ni urithi muhimu unaopaswa kulindwa na kuendelezwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Wameongeza kuwa kupitia mazungumzo ya wazi, kuheshimiana na kujenga maridhiano, Tanzania itaendelea kusonga mbele ikiwa imara zaidi, huku ikidumisha utulivu na mshikamano wa wananchi wake.