Katika ramani ya kimkakati ya kuelekea Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050, hakuna mkoa unaoakisi kwa vitendo maana ya “Amani ni Kiini cha Ukuaji wa Uchumi” kama unavyofanya mkoa wa Mwanza hivi sasa. Wakati mataifa mengi duniani yakihangaika kutafuta utulivu wa ndani, wakazi wa mkoa huu wa kimkakati nchini Tanzania wanashuhudia jinsi amani imekuwa mtaji namba moja unaoendesha ukuaji wa Pato la Mkoa (GDP) kwa kasi ya ajabu.
Hii si bahati mbaya, bali ni matokeo ya uwiano thabiti kati ya maono ya Serikali ya Awamu ya Sita na utendaji bora wa vyombo vya ulinzi na usalama. Vyombo hivyo vimefanikiwa kudhibiti uhalifu kwa kiwango cha kuridhisha, na kuufanya mkoa wa Mwanza kuwa kimbilio salama la wawekezaji wa ndani na wa nje.
Uwiano huu unaonekana wazi katika miradi mikubwa ya mabilioni ya shilingi inayotekelezwa mkoani, kuanzia ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) hadi Daraja la J.P. Magufuli. Miradi yote hii inategemea utulivu wa kijamii ili ikamilike kwa wakati. Kuanzia wavuvi wa Ziwa Victoria hadi wafanyabiashara wa Soko la Mwaloni, wananchi wa Mwanza kwa kauli moja wanakiri kwamba amani imeongeza mzunguko wa fedha na kuunda ajira nyingi, hasa katika sekta isiyo rasmi.
Bila ulinzi madhubuti wa maisha na mali, hata mipango mizuri zaidi ya maendeleo ingebaki kuwa ndoto tu. Hofu ni adui mkubwa wa uzalishaji. Viongozi wa kijamii na wananchi wa kawaida wamebainisha kuwa kufanya kazi saa 24 sasa imekuwa ni kawaida, jambo linalochangia kwa kiasi kikubwa kuongeza mapato ya serikali kupitia kodi na tozo mbalimbali.
Ufanisi wa vyombo vya usalama umeleta matokeo ya moja kwa moja , Mwanza sasa inajivunia mazingira rafiki zaidi kwa biashara, huku visa vya uporaji na uvunjifu wa amani vikishuka kwa kiwango cha kihistoria. Hili ni fanikio la kizalendo ambalo linastahili kuenziwa, kwani amani ni tunda ambalo kila mtu anafaidika nalo; mama lishe anauza chakula chake kwa utulivu, na mwekezaji wa kiwanda anazalisha bidhaa zake bila hofu yoyote.
Hata hivyo, ujumbe mzito kutoka kwa wananchi wa Mwanza kwa Watanzania wote ni huu: “Amani ni kama hewa” huwa huioni umuhimu wake mpaka inapokosekana. Wanasema bila amani, kila mtu ataathirika, na maendeleo yote yaliyopatikana yanaweza kupotea kama moshi.
Kwa kuipongeza serikali na vyombo vya dola, wakazi wa Mwanza wameonyesha ukomavu wa kizalendo wa hali ya juu. Wanatambua kwamba jukumu la kulinda amani ni la kila mtanzania. Utalivu huu si mafanikio ya serikali pekee, bali ni ushindi kwa kila raia anayetamani kuona taifa lake likipiga hatua kuelekea uchumi wa kisasa na jumuishi.